Pages

JOSEPH KANIKI NA MATUMLA NJEE KWA DHAMANA SASA WAKATA MITAA TU ETHIOPIA.



STRAIKA wa zamani wa Simba, Joseph Kaniki ‘Golota’ na bondia chipukizi, Mkwanda Matumla waliokuwa mikononi mwa polisi jijini Addis Ababa, Ethiopia kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya wameachiwa kwa dhamana.

Watuhumiwa hao wawili ambao wanajuta kwa kitendo kilichowakumba walipewa dhamana Ijumaa iliyopita na kutakiwa kulipa Birr za Ethiopia 30,000 (Sh.2.6 milioni) jana Jumatatu.

Ingawa Kaimu Balozi wa Tanzania, nchini humo, Samwel Shelukindo hakupokea simu jana Jumatatu kutoa ufafanuzi kuhusu hilo, lakini Mwanaspoti linaweza kuthibitisha kwamba wachezaji hao walilipiwa faini hiyo na kuingia mtaani.




“Hakuna mtu aliyewahi kuomba dhamana kwenye tuhuma kama hizo, ndiyo maana hata wale Watanzania wengine walikaa ndani mpaka baadaye wakafungwa na kumaliza kifungo chao. Lakini kumbe kisheria kuna jinsi ya kutafuta dhamana ndio maana ubalozi ukawasaidia wakapata dhamana lakini kwa masharti makali ya kulipa Birr 30,000 sawa na dola 1,800 za Marekani,” kilidokeza chanzo cha uhakika jana Jumatatu.

“Ile Ijumaa hawakuweza kulipa hizo fedha ndio maana leo (Jumatatu) ubalozi ukakamilisha taratibu wakatoka, lakini hawataruhusiwa kutoka nje ya hapa Addis Ababa. Tunawafanyia utaratibu wa kuwatafutia makazi ya muda, tuangalie utaratibu wa kesi yao ukoje.

“Kwavile mambo ni magumu, ikumbukwe kwamba hapa walikuwa wanapita tu hawakuwa na viza, hivyo hata kama wanataka kutoka nje ya hapa haiwezekani na wala hawawezi kuendelea kukaa hapa mpaka tuwafanyie utaratibu wapate viza, lakini hayo yote yatakamilishwa na ubalozi,” kilisema chanzo cha kuaminika.

Habari za ndani zinasema kwamba wachezaji hao watakaa kwa muda Addis wakati taratibu za kesi yao zikiendelea chini ya polisi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai.

Wanamichezo hao walidaiwa kukamatwa na kilo saba za dawa za kulevya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa. Mkwanda alidaiwa kukutwa na kilo nne wakati Kaniki alidaiwa kukutwa na kilo tatu.

Ilidaiwa walikuwa wanajiandaa kuunganisha ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kwa ajili ya kwenda Paris, Ufaransa.

Awali ilidaiwa kwamba wanamichezo hao waliwaeleza polisi kwamba walikabidhiwa mizigo hiyo na mtu mmoja baada ya kupita sehemu zote za ukaguzi kwenye Uwanja wa Ndege wa Mombasa, Kenya.

0 comments:

Post a Comment