Sumbawanga. Siyo jambo geni kusikia wanawake wakiwalalamikia wauguzi ama kwa kuwapiga au kuwatukana wakati wa kujifungua.
Hata hivyo, matukio ya mama kupoteza maisha ama
mtoto aliye tumboni kufariki kwa ajili ya vitendo hivyo vimekuwepo,
lakini siyo kwa wingi.
Rehema Michael (18), mkazi wa Kijiji cha Tentula
Sumbawanga Vijijini ni mmoja kati ya waliokutana na chungu ya kutukanwa
na kupigwa na muuguzi wakati wa kujifungua.
Rehema ambaye ilikuwa ni mimba yake ya kwanza, amepoteza mtoto na yeye mwenyewe kunusurika kifo kutokana na hali yake.
Rehema akiwa mchovu anasimulia kwa uchungu kisa chote tangu alipopata uchungu wa kujifungua mpaka alipofikishwa hospitali.
“Nilisikia uchungu siku ya Jumatatu, nikamwambia mama mkwe ,tukaondoka naye kwenda kwenye zahanati ya pale kijijini Tentula.
“Tulipofika hatukumkuta muuguzi wa zamu na daktari
tuliyemkuta hakuwa na funguo ya chumba kwa hiyo akatubeba kwenye
pikipiki mpaka kwenye kituo cha afya cha Ikozi.
“Nilipofika hapo nikaingizwa kwenye chumba cha
kuzalia, nikawa najitahidi kusukuma mtoto, nesi akanipiga ili nisukume
mtoto, nilijitahidi kusukuma mtoto mpaka kichwa kikaanza kutoka hadi
kufikia kidevu, lakini kwa kuwa nilivyokuwa napigwa nikaishiwa nguvu.
Muuguzi akaniambia niache uvivu, “Sukuma, acha
ujinga, nani alikutuma?” akaendelea hivyohivyo, kwa kweli nilikuwa
nasikia maumivu sana.
Nilipoishiwa nguvu aliendelea kunipiga ili
nisukume mtoto, lakini nikashindwa ndiyo ikabidi gari liitwe ili niletwe
hapa kwenye hospitali ya mkoa.
Nilifika huko mtoto akining’inia, hivyo mpaka
ninafika hapo, nilipotoka huko mpaka mtoto alikuwa hai, lakini mpaka
nafikikishwa hapo, nikaambiwa mtoto ameshakufa.
