Nairobi. Kocha wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amesema mipira ya juu pamoja na Uwanja wa Kenyatta uliopo Machakos kujaa maji ndiyo kilichoifanya timu yake kushindwa kuisulubu Zambia.
Stars ilitoa sare ya bao 1-1 na Zambia kwenye
mechi yake ya kwanza ya kundi B ambayo ilitoa nafasi kwa Burundi
iliyoichapa Somalia mabao 2-0 kuongoza kundi.
Poulsen alisema,”Kipindi cha kwanza tulikuwa
tunapiga mipira mirefu ile siyo staili yetu, ndiyo maana timu ilishindwa
kucheza mpira mzuri.”
“Hata sura nyingi mpya kwenye kikosi cha kwanza
zilifanya staili ya mchezo kubadilika na hali ya uwanja pia, lakini
ikabidi kipindi cha pili tuingie na mikakati mipya ambayo ilisaidia
tukatuliza mpira chini na mambo yakaonekana, ingawa bado tulikosa nafasi
nyingi za kufunga,”alisema.
Kocha huyo hakulaumu mchezaji yeyote, lakini
aliahidi kufanya mabadiliko kadhaa kwenye kikosi kitakachocheza na
Somalia Jumapili kwa vile ushindi ni lazima.
“Lazima tufanye mabadiliko kutokana na staili ya
mchezo na ushindi unatakiwa,”alisisitiza Poulsen huku akimsifu kipa
wake, Ivo Mapunda kwa kucheza mipira ya juu.
Stars walilazimika kucheza mipira ya juu katika
kipindi cha kwanza cha mechi ya Zambia kutokana na maji yaliyokuwa
yamejaa uwanjani ambayo yalikuwa yakipunguza kasi ya mchezo na
kusababisha wachezaji kutumia nguvu nyingi hususani viungo.
Stars ina pointi moja kwenye kundi lake sawa na Zambia yenye straika Felix Katongo.
0 comments:
Post a Comment