Pages

ZIDANE: HAPANA BALE HAWEZI AKAUZWA KWA BEI HIYO BADO HANA KIWANGO CHA HIVYO.














MADRID, HISPANIA

HAKUNA mchezaji mwenye thamani ya Pauni 85 milioni. Hata Gareth Bale hana thamani hiyo. Ni Zinedine Zidane ndiye anayeamini hivyo.

Amefunguka na kuweka wazi kilicho moyoni kwake kuhusu uhamisho wa Bale kutoka Tottenham Hotspurs.

Bale amejiunga na Real Madrid kwa uhamisho wa Pauni 85 milioni zilizovunja rekodi ya uhamisho ya Dunia akisaini mkataba wa miaka sita Santiago Bernabeu.

Kwa kiwango hicho cha pesa, Bale, amevunja rekodi ya uhamisho ya Cristiano Ronaldo aliyesajiliwa kwa uhamisho wa Pauni 80 milioni akitokea Manchester United mwaka 2009.

Lakini Zidane ambaye aliwahi kuvunja rekodi ya uhamisho mwaka 2001 alipojiunga kwa uhamisho wa Pauni 56 milioni kutoka Juventus kwenda Madrid, haamini kama viwango vya pesa ni sahihi.

Zidane anaamini kuwa ada yake ya uhamisho ilikuwa kubwa na haikustahili na anashangazwa kuona mchezaji kama Bale anaweza kugharimu kiasi hicho cha pesa katika wakati kama huu ambapo uchumi wa dunia unayumba.

“Inabidi ujiulize swali hilo kila mara. Miaka kumi iliyopita walininunua mimi kwa Euro 75 milioni na nilisema sikuwa na thamani hiyo. Sasa nasema mchezaji (Bale) hana thamani hiyo. Tatizo klabu mbili zinakubaliana na hakuna anayeweza kulazimisha vinginevyo,” alisema Zidane ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi wa kocha mpya wa timu hiyo, Carlo Ancelotti.

“Hilo ndio soka, bahati mbaya inasikitisha kuona kinachotokea sasa. Watu wanalipa pesa nyingi sana.”

Hata hivyo, Zidane anaamini kwamba Bale ana kila sababu ya kuibuka mchezaji mahiri zaidi Santiago Bernabeu na yuko tayari kumpa kila aina ya msaada anaoutaka akiwa kama kocha wake.

“Jukumu langu litakuwa kumwambia acheze kama anavyojua, asijiweke katika presha. Ana kipaji kizuri lakini bado ana nafasi ya kuimarika zaidi,” aliongeza Zidane ambaye aliiongoza Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia katika ardhi yao mwaka 1998.

Bale ambaye kwa sasa yupo katika majukumu ya timu ya taifa lake la Wales, anatazamiwa kuichezea Real Madrid pambano lake la kwanza mnamo Septemba 14 wakati watakapokipiga dhidi ya Villarreal katika pambano la Ligi Kuu Hispania.

0 comments:

Post a Comment