Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta amekiri “kuchezewa” kwa saini ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na sehemu ya saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa zilizopo kwenye hati ya sheria ya kuridhia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Akizungumza na gazeti hili jana, Sitta alisema ni 
kweli kuna maneno katika hati hiyo ya sheria namba 22 ya 1964, 
iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa, Aprili 25, 1964, yameongezwa.
Alisema katika saini ya Nyerere kumeongezwa herufi
 “us” kwa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa kumeandikwa neno 
“Msekwa” kwa kompyuta, jambo ambalo ni makosa. Sitta alisema walioongeza
 maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali 
baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini 
walifanya makosa.
“Wale vijana walipoona document (nyaraka) 
haisomeki waliongeza “us” mwisho kwa kompyuta kwenye saini ya Nyerere, 
ila walifanya makosa maana bora kitu kionekane kufifia hivyo hivyo 
lakini kibaki na maana yake,” alisema.
Hata hivyo, Sitta alisema kwa waliofanya kazi na 
hayati Baba wa Taifa wanatambua saini iliyopo kwenye hati ya sheria hiyo
 ipo sawa ukiondoa makosa ya kuwekwa herufi hizo.
Kuhusu saini ya Msekwa, alisema pia kulifanyika makosa katika sehemu ya saini hiyo, kuandikwa kwa kompyuta “Msekwa”.
“Ni saini ya Msekwa, lakini vijana wa chamber kwa 
AG waliongeza neno “Msekwa” kwa kompyuta. Ni mtu asiyejua thamani na 
uhalisia wa saini ni kubaki ilivyo hata kama kwa miaka 100 hata mtu aje 
kuisoma kwa darubini,” alisema.
Hata hivyo, alisema maudhui ya hati ya sheria 
hiyo, iliyosainiwa rasmi Aprili 25, 1964 ni sahihi kama ambavyo 
walikubaliana waasisi wa Muungano, Nyerere na Karume.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa
 Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alisema kwamba hafahamu kama ofisi
 yake inahusika na kuchezewa kwa saini hizo, tofauti na madai ya Sitta.
Sheria iliyopitishwa Z’bar
Sitta alisema ili kuondoa utata, ameagiza kupatiwa
 hati ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume (Presidential Decree) 
aliyotoa kusaini makubaliano kwani wakati huo, hakukuwa na Bunge.
“Karume alitumia Baraza la Mapinduzi akatumia amri
 ya Rais akasaini. Tunatarajia kuipata hiyo, sasa tutakuwa tumepata 
nyaraka za Bara na Zanzibar,” alisema Sitta.
