London, England. Barcelona wanaonekana wamerudi katika kiwango chao katika muda sahihi wakijiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa hatua ya 16 bora dhidi ya Manchester City leo kwenye Uwanja wa Etihad.
Baada ya kushinda mechi moja kati ya nne za La Liga, pamoja na kipigo cha kushangaza nyumbani dhidi ya Valencia, lakini vijana wa Catalan wameshinda mechi mbili za karibuni wakifunga mabao 10.
Walishinda 4-1 dhidi ya Sevilla wiki iliyopita na Jumamosi walichakaza Rayo Vallecano 6-0 na kuendelea kuongoza ligi kwa tofauti ya mabao kwa Real Madrid na Atletico Madrid.
Katika mechi hiyo walipata mabao kupitia Neymar, huku bao la nne likigongwa pasi kabla ya Pedro Rodriguez kufunga, wakicheza kwa mfumo wa enzi za Barcelona ya Pep Guardiola.
Guardiola sasa yuko Bayern Munich, ambayo ilisambaratisha Barca 7-0 katika nusu fainali ya michuano hiyo msimu uliopita, lakini klabu yake ya zamani imejiimarisha zaidi baada ya kufuzu kwa fainali ya Kombe la Mfalme kwa kuitoa Real Sociedad.
“Sasa tupo kwenye kipindi muhimu cha msimu, kila mechi ni muhimu kwetu,” nahodha Carles Puyol aliimbia Barca TV.
“Tulicheza vizuri dhidi ya Rayo, kama ilivyokuwa dhidi ya Real Sociedad na sasa timu imeongeza kujiamini kwake.
City wanawahofia wapinzani wao wanaokutana kwa mara ya kwanza kwenye hatua ya mtoano, lakini kikosi cha Manuel Pellegrini kimepata faraja baada ya matokeo ya mwishoni mwa wiki.
Baada ya kucheza mechi mbili bila ya ushindi, mabingwa wa England 2012, walionyesha soka ya kiwango cha juu Etihad wakiichapa Chelsea 2-0 katika raundi ya tano ya Kombe la FA.
Ushindi huo ni kisasi baada ya kufungwa 1-0 na Chelsea katika Ligi Kuu siku 12 zilizopita na Samir Nasri anaamini ushindi huo ni maandalizi mazuri kwao kuwakaribisha Barcelona.
“Ni mechi ngumu,” alisema kiungo huyo wa Ufaransa ambaye alicheza kwa mara ya kwanza baada ya kukaa nje kwa wiki tano akiuguza majeraha ya goti.
“Kila mchezaji anataka kucheza aina hii ya mechi katika Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona. Jambo zuri kuwa tupo imara na tunajiamini vya kutosha.