Pages

SOKA :EMANUEL OKWI OLOYA WAMTOA KAFARA DHAIRA.





HUENDA kufikia Januari mwakani, Juma Kaseja akawa katika lango la Simba, Emmanuel Okwi na Mosses Oloya wakawa mawinga wa Simba, mmoja akicheza kulia na mwingine kushoto.

Ni endapo tu kama kundi moja la uongozi litashinda katika ubishi unaoendelea kwa siri miongoni mwao katika barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Uongozi wa Simba umegawanyika katika makundi mawili, huku kila upande ukivutia upande wake.

Kundi la kwanza linataka kumrudisha kipa aliyejenga heshima na Simba, Juma Kaseja klabuni huku likitaka kipa wa sasa, Abel Dhaira aondolewe na nafasi yake ijazwe na wachezaji wawili wa kigeni, Okwi na Oloya.

Mpaka sasa ina wachezaji wanne wa kigeni; Dhaira, Amis Tambwe, Gilbert Kaze na Joseph Owino hivyo ina nafasi moja tu kuongeza mchezaji wa kigeni na ndiyo maana kundi la kwanza linataka Dhaira atemwe ili wawaongeze Oloya na Okwi.

Hata hivyo, wazo la Kaseja kurudi katika lango la Simba linapingwa na kigogo mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba pamoja na baadhi ya watu ndani ya benchi la ufundi kwa madai ataigawa timu.


Kuna makundi mawili ambayo yanapingana kuhusu kumchukua tena Okwi, huku kundi moja likidai kwamba staa huyo ana maringo na ni msumbufu katika kuivaa jezi ya Simba licha ya umahiri wake.

Kundi hilo linadai kuwa Okwi hana nidhamu, kwa sababu anapokwenda kwao Uganda huwa anakaa muda mrefu bila sababu yoyote na huzima siku yake.

“Huwa hataki kuwepo wakati wa mazoezi ya mwanzo wa msimu, timu ikiwa kambini anachelewa, kwa jumla ni msumbufu. Unaona sasa yupo Uganda tangu Juni wakati timu yake ya Etoile du Sahel inamhitaji Tunisia,” kilisema chanzo chetu kutoka Msimbazi. Kundi lingine linaloongozwa na kiongozi mwingine wa zamani wa klabu hiyo linadai kwamba Okwi ni mchezaji muhimu klabuni na ataimarisha safu ya ushambuliaji ya Simba akishirikiana na straika mwenye uchu wa mabao Amisi Tambwe na Betram Mwombeki.

Mwanaspoti linajua kwamba Okwi ambaye alikuwa Dar es Salaam siku chache zilizopita amefanya mazungumzo na baadhi ya vigogo wa Simba kuhusiana na hatma yake lakini wakakubaliana wasubiri kwanza waangalie deni wanaloidai Etoile du Sahel kama litalipwa wikiendi hii na kama litashindikana waone Fifa itaamua nini.

Simba kwa sasa wanajaribu kukwepa kabisa kujihusisha na Okwi kwa sababu wanajua kuwa Etoile du Sahel inaweza kuchukulia kigezo hicho na kukataa kulipa fedha za kumnunua Sh480 milioni.

Ingawa Edgar Agaba ambaye ni mwanasheria wa Uganda aliyetuma vielelezo vya Okwi Fifa wiki iliyopita kutaka mkataba wa mchezaji huyo na Etoile usitishwe awe huru, habari zinasema amefanya mazungumzo na SC Villa ya Kampala na ndiyo iliyoko mstari wa mbele kuhakikisha mkataba huo unavunjwa.

0 comments:

Post a Comment