skip to main |
skip to sidebar
ULINZI anaopatiwa Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania,
Sheikh Issa Ponda, akiwa mahabusu ndani ya Gereza la Segerea, Dar es
Salaam, ni mkali na umeelezwa kuwa ni mara mbili ya ule aliokuwa
akipatiwa awali wakati alipokuwa hapo, MTANZANIA Jumapili limedokezwa.
Chanzo cha habari cha gazeti hili kilicho ndani ya gereza hilo,
kilieleza kuwa ulinzi wa Sheikh Ponda umeimarishwa mara mbili zaidi
kutokana na sababu za kiusalama.
Ulinzi ulioongezwa ni pamoja na ule wa maaskari magereza
wanaomlinda, lakini pia vimeongezwa vikwazo ili kuwazuia watu kumuona
ovyo.
Ni katika hali hiyo ya kuimarisha ulinzi dhidi ya kiongozi
huyo, gazeti hili limedokezwa kuwa, hivi sasa Sheikh Ponda anaelezwa
kulala katika chumba maalumu peke yake.
Akiwa mahabusu katika
gereza hilo, mwaka jana kabla hajahukumiwa kifungo cha nje cha mwaka
mmoja, Sheikh Ponda inadaiwa alikuwa akilala katika chumba maalumu,
lakini wakiwa wawili yeye pamoja na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa
Chadema, Wilfred Lwakatare.
Lwakatare kwa sasa yuko nje kwa dhamana, kutokana na kesi inayomkabili ya kula njama ya kutaka kudhuru kwa sumu.
Habari
zilizolifikia gazeti hili, zinaeleza kuwa katika kuhakikisha usalama wa
Sheikh huyo, hairuhusiwi mtu yeyote kumwona pasipo ruhusa kutoka ndani
ya familia pamoja na kibali kutoka katika uongozi wa Magereza.
“Kwanza
kwa sasa analala ‘special room’ (chumba maalumu), yaani fresh kabisa na
ukitaka kumwona mpaka uidhinishwe na familia kutokana na ulinzi
ulivyoimarishwa, chakula chake anachokula analetewa na ndugu zake pamoja
na mke wake, cha hapa labda siku akipenda,” kilisema chanzo hicho.
Ni
kwa namna hiyo ya kuimarisha ulinzi kwa Sheikh Ponda, takribani zaidi
ya wiki mbili zilizopita serikali ilijikuta ikitoboka mfuko kwa kutumia
kiasi cha Sh milioni 10,682,031 kama gharama za usafiri wa helikopta za
kumpeleka na kumrudisha mahakamani mkoani Morogoro, katika kesi ya
uchochezi inayomkabili.
Sheikh Ponda, ambaye anaelezwa kuigharimu serikali kiasi chote hicho cha fedha, ukiachana na gharama nyingine,
alikamatwa
hivi karibuni na kurudishwa Segerea kwa mara ya pili akiwa bado
anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja kwa kosa la uchochezi.
Ingawa
taarifa rasmi hazijathibitishwa, Ponda anadaiwa kupigwa risasi akiwa
katika harakati za kuondoka katika Mkutano aliofanya Morogoro, ambapo
mpaka sasa anauguza jeraha katika mkono wake wa kulia.
Hata
hivyo, kesi yake hiyo ya kwanza ilifutwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu na kufunguliwa nyingine mkoani Morogoro, anakotuhumiwa kuwa
Agosti 10, mwaka huu, katika eneo la Uwanja wa Ndege, aliwaambia
Waislamu wasikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti,
kwa madai kuwa zimeundwa na BAKWATA, ambao ni vibaraka wa CCM na
serikali.
Pia anadaiwa kuwaagiza waumini hao kuwa endapo watu hao
watajitokeza kwao na kujitambulisha kwamba ni kamati za ulinzi na
usalama za misikiti, wafunge milango na madirisha wawapige.
Ilielezwa
kuwa kauli hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, iliyotolewa na Hakimu V. Nongwa Mei 9, mwaka huu, ambayo
ilimtaka Ponda ndani ya mwaka mzima kuhubiri amani.
Katika
shitaka la pili, anadaiwa siku hiyo hiyo katika eneo la Uwanja wa Ndege,
Morogoro, Ponda aliwaambia Waislamu kuwa serikali ilipeleka jeshi
Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi ili kuwaua,
kuwabaka na kuwatesa wananchi, kwa sababu asilimia 90 ya wakazi hao ni
Waislamu.
Kwamba, serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa
Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji
baada ya kudai ni mali yao, kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wa huko ni
Wakristo.
Katika shitaka la tatu anadaiwa kuumiza imani za watu
wengine kinyume cha kifungu cha sheria namba 390 na kanuni ya adhabu
namba 35 cha mwaka 2002.
Hata hivyo, Sheikh Ponda ameyakana mashtaka hayo na kukubali baadhi ya vipengele.
0 comments:
Post a Comment